Ad Code

Mkude Ahamishiwa Hospitali ya Muhimbili

KIUNGO mkabaji wa Simba, Jonas Mkude amehamishiwa kwenye Hospitali ya Muhimbili akitokea Hospitali ya Rabininsia Memorial ya Tegeta ili kuhakikisha anarejea haraka uwanjani kuipambania timu yake.

Kiungo huyo alipata majeraha katika vidole viwili vya mguu wa kulia baada ya kukanyagwa na beki wa kulia wa KMC, Kelvin Kijili wakati timu hizo zilipocheza mchezo wa kirafiki.

Timu hizo zilivaana juzi Jumatatu kwenye Uwanja wa Simba Mo Arena, Bunju nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam mchezo ulipomalizika kwa Simba kushinda mabao 3-1.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Daktari wa Simba, Yassin Gembe alisema kiungo huyo anaendelea na matibabu Muhimbili akiwa nje ya uwanja akiuguza majeraha hayo.

Gembe alisema kuwa, kiungo huyo hivi sasa amepata nafuu kidogo ya majeraha yake hayo aliyoyapata huku akiamini kurejea kwa haraka uwanjani kuipambania timu yake katika michezo ya ligi waliyoibakisha na Kombe la FA.

“Mkude anaendelea vizuri baada ya kupata majeraha kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya KMC tuliocheza Jumatatu iliyopita ambao alishindwa kumalizia mchezo huo kutokana na majeraha.

“Baada ya kupata majeraha hayo, haraka tulimkimbiza hospitalini kwa ajili ya kumpa huduma ya kwanza katika Hospitali ya Rabininsia Memorial iliyokuwepo Tegeta, Dar kwa ajili ya kupatiwa huduma ya kwanza.

“Lakini hivi sasa tumemuhamishia Hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu ya kufanyiwa vipimo suala la lini atarejea uwanjani ni siri lipo chini ya uongozi,” alisema Gembe.
Stori: Wilbert MolandiDar es Salaam
Reactions

Ad Code

Responsive Advertisement